JINA LA KITABU: KIROBA CHEUSI
AINA YA KITABU: RIWAYA
JINA MWANDISHI: LAURA PETTIE
NCHI: TANZANIA
MWAKA WA KUCHAPISHWA: 2019
KUHUSU KITABU
KIROBA CHEUSI...
Morena binti hohehahe anashawishiwa na shoga yake, Fatumata, kukiiba kiroba cheusi kilichosheheni almasi. Waliamini hiyo ndiyo ingekuwa njia pekee ya kuuaga umasikini uliowaelemea.
Ni mpaka pale hii ndoto yao ya utajiri wa haraka ilipogeuka kuwa jinamizi la kutisha. Wanabaini kumbe wamecheza patapotea na kukichokoza kifo chenye uchu.
Kinachofuatia ni saa 72 za kufa na kupona, wanajikuta wakihaha huku na huko, usiku na mchana, mjini na msituni, katika mchakamchaka wa kunusuru uhai wao.
Katikati ya sakata zima, wanakutana na Mzee Shata anayewapa ahadi ya kuwanusuru na kifo. Lakini, ghafla wanagundua kumbe wameingizwa mjini, na sasa wana kazi ya kupambana na kisanga kingine tena ndio wanusurike, ilhali muda ukizidi kuwatupa mkono.
Wanaangukia mikononi mwa kijana jamali Tarik Dizzo. Hapa mchakamchaka unaowagharimu machozi, jasho na damu unaingia kwenye mtanziko mkubwa unaomlazimu Morena kuamua kati ya utajiri, mapenzi na uhai… kipi kina thamani zaidi kwake?
KIROBA CHEUSI ni simulizi inayosisimua sana.
Ikiwa imesheheni visa na mikasa ya kuogofya, kuchekesha na taharuki za kushtukiza. Huku ikijikita kwenye thamani ya urafiki wa kweli, mapenzi na usaliti.
Inafunza kuhusu maisha, matabaka kwenye jamii, uwepo wa Mungu maishani mwetu na mitihani inayotukabili kila siku.